Siku ya Wanawake Duniani - 2019


Siku ya Wanawake Duniani - 2019

Leo ni siku ya wanawake duniani; siku ambayo dunia nzima inamsherehekea na kumfurahia mwanamke, na pia kuangazia maswala yanayomkumba mwanamke. Kwa hivo nachukua fursa hii kujiunga na watu wote wenye heri njema duniani kuwatakia wanawake wote siku njema.

Mwanamke Ni Nani?

Jibu la swali hili linafaa kuwa rahisi tu, mwanamke ni mwanamke! Lakini sivyo, mwanamke si tu mwanadamu anayezaliwa na uke bali ni mwanadamu mwenye hulka za kike zinazokubalika katika jamii. Mwanamke si mtoto wa kike tu, bali ni mtoto anayefanya mambo yanayopelekana na uke. Katika dunia ya sasa imekuwa vigumu kumtambua mwanamke kwa vile anavyoiga mitindo ambayo wazee wetu hawakuyaona kwa wake zao. Lakini hilo si hoja, hivi leo tutaangazia mwanamke kama mwanadamu wa kike kisha tuangalie hulka zake na tutaje yale yasofaa na yale yanayofaa - kwa maoni yangusmiley.

Majukumu na Hulka Za Mwanamke

Mwanamke ana majukumu mengi mno katika jamii. Mwanamke anafaa kuamka asubuhi na mapema ili kuwatayarisha wanawe pamoja na mumewe iwapo ana mume. Mwanamke pia anafaa kuingia nyumbani mapema ili kuitayarishia jamii yake chajio kwa wakati ufaao. Mbali na hayo, mwanamke anafaa kuhakikisha mambo ya nyumbani yapo sawa kila wakati. Anafaa pia kumsaidia mume katika shughuli zote za pale nyumbani.

Nyakati zimebadilika sasa na wanawake wamekuja na mambo mengine ambayo hayakuwa zamani. Wanaume wameteta sana kuhusiana na mambo ya kisasa yanavyoadhiri wanawake lakini naona ni vyema pia sisi kama waume tukubali mambo mengine;

♦Zamani mwanamke alikaa nyumbani wakati wote na kumngojea mumewe atafute alete. Siku hizi mwanamke anatoka pamoja na mumewe wakielekea kazini. Kwa hivyo wanawake wamepungukiwa na muda wa kufanya shughuli zingine za nyumba. Hata hivyo, mwanamke lazima ajikaze zaidi ili aweze kufanya mambo mengine ya nyumbani bila kusema eti kazi imemzuia.

♦Wanawake wa zamani hawakuruhusiwa kuketi katika mabaraza ya wazee au kushikilia nafasi za uongozi. Hata makanisani wanawake hawakushikilia nyadhfa kuukuu za uongozi. Siku hizi wanawake wanaongoza si tu katika makanisa na katika siasa bali pia katika makampuni. Kuna wanawake wengi ambao ni maafisa wakuu watendaji wa kampuni kuukuu nchini. Hilo hatufai kulipinga.

♦Hapo kale mwanamke alikuwa mali ya mumewe kama vile ng'ombe au panga. Mwanamme angemtumia atakavyo na hata kumtimua wakati wowote. Tusiwalaumu waume wale kwa sababu mwanamke alikuwa ananunuliwa kwa ng'ombe wengi mno. Hivi sasa wanawake wanaheshimiwa na wanausemi katika jamii.

Hulka Zisizofaa

⇒ Tabia ya kujiita mwanamke huru (independent woman); mwanamke katika wakati wowote maishani mwake anawezakuwa pekee, anapanga kufunga ndoa, ameolewa, ametalikiwa, au mjane - amefiwa na mumewe. Hakuna binadamu huru. Kuna msemo usemao kwamba;

Mwanadamu si kisiwa

Mwanamke huru ni yule ambaye haitaji marafiki, wazazi, watoto, au kitu chochote kinachoweza kumsaidia. Pesa pekee hazitoshi kumpa mtu uhuru; bado unahitaji marafiki na mambo mengine. Lakini pia mwanamke wa kisasa anawezakaa bila kuolewa na ni hawa wanaopenda kujiita huru; uhuru huo unalinganishwa na kutokuwepo kwa mume maishani mwao. Sidhani hilo pekee linatosha; na hata wakati mwingine wanawake hawa huwa na jamaa kule chinichini wakifurahisha miili yao kisha wanatokea katika mitandao ya kijamii kusema wako huru. Ni vyema mtu aelewe hali yake na aikubali na aishi bila kujidanganya.

Adui wa mke ni mke; lakini mbona iwe hivi kila wakati? Wanawake hupigana vita wenyewe kwa wenyewe. Hawatakiani mema. Mmoja akifanikiwa wengine wasema ameinuliwa na mwanamme. Hawapigani jeki maishani wanawake. Najua kuna wengine hujaribu ila bado kuna mengi mwawezafanya. Ningependa kuona wanawake wa kisasa wameshikana, wanainuana kwa hali na mali na kusaidiana. Hatuhitaji sheria za kusawazisha jinsia ikiwa wanawake wanawezashikana na kusaidiana. Wakati mwingine wao ndio wengi.

Adui wa mke ni mke

⇒ Mambo mengine ni kama kuiga, mavazi yasopendeza, na kupoteza wakati. Kupoteza wakati kunatokea pale ambapo wanawake wanajihusisha na mambo ya vitina na mengine ambayo yanawapotezea wakati mwingi. Sina mengi ya kusema hapo; wanawake mna mengi ya kufanya nyumbani kwa hivyo msichukue wakati mwingi kufanya yale mengine.

Pale kwa mavazi natarajia kupingwa sana. Wanawake wanasema;

Mavazi yetu; chaguo letu

Lakini sikubaliani na hilo. Wanawake wengi (si wote) huvaa mavazi ili yapendeze. Ndio maana ukiambiwa, "mavazi yako yapendeza." unatabasamu na usipoambia unahisi vibaya. Kuna mavazi ambayo hayakubaliki katika jamii. Chagueni mavazi yanayoambatana na mambo mnayotenda na mahali mwendapo. Hilo tumelisema mara mia na wengine wameshasikia.

Tabia ya kuiga ipo kwa wanawake. Amtembelea rafikiye kisha anarudi akisema mwenzake ana shuka nzuri kwa hivo analitaka pia. Wengine wanawapa waume wao wakati mgumu wakitaka kufanyiwa yale ambao waume wa rafiki zao wamewafanyia hao rafiki zao. Hili pia liangaliwe.

Uwezo wa Mwanamke

Tutamalizia hapa, lakini kabla ya kikomo chenyewe, ni vyema niwakumbushe dada na mama zetu kwamba mna uwezo mkubwa katika jamii ingawa wakati mwingine mnasahau. Ninyi ndio shingo ya nyumba; mnashikilia kichwa cha nyumba - mume - kisianguke. Mna uwezo wa kukipindua kichwa kiangalia panapofaa. Ninyi ndio mnapanga jamii. Ninyi ndio mnakaa na wanenu kwa muda mrefu. Jamii pia inaendelea kuwapa nafasi mbalimbali. Tumia nafasi na uwezo mnaopata kusaidia jamii, kuinuana, kuheshimu waume zenu, na kunyenyekea. Mwisho kabisa, someni Biblia au Quran ili muweze kuongoza jamii kulingana na mafunzo ya kidini. Nawaachia neno hili;

Msiige tabia na mienendo ya dunia hii bali mbadilishwe, nia zenu zikifanywa kuwa mpya, ili mpate kuwa na hakika ni nini mapenzi ya Mungu: yaliyo mema, yanayopendeza machoni pake na makamilifu. (Warumi 12:2).

Posted 2019-03-08 10:47:14 | 585
Posted by Fred Barasa Makokha Fred Barasa Makokha Admin

Whoops, looks like something went wrong.